Kuhusu WWF
Taasisi ya Wapo Wapi Foundation (WWF) ni shirika lisilo la kiserikali lililoanzishwa mwaka 2023, lenye dhamira ya kushughulikia suala la upotevu wa watoto nchini Tanzania. Jina lake, “Wapo Wapi,” linatokana na neno la Kiswahili linalomaanisha “Where are they” kwa Kiingereza, likiashiria swali la machungu ambalo mara nyingi wazazi na familia za watoto waliopotea hujiuliza. Shirika hili limesajiliwa chini ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2002 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na limepewa namba ya usajili 00NGO/R2/4311.
Lengo kuu la taasisi ni kutoa msaada wa kijamii na kisheria kwa familia zinazopitia changamoto za kupotelewa na watoto, pamoja na kufanya kampeni za uhamasishaji na kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali ili kupunguza tatizo la upotevu wa watoto nchini.
- Tunafanya Mabadiliko
Tunatumika kama taa ya matumaini kwa watoto na familia zao kwa kutoa usaidizi wa kimsingi. Kupitia huduma mbalimbali tunazotoa, tunafanya kazi bila kuchoka kupunguza idadi ya watoto wanaopotea, kuongeza nafasi za kuwapata, na kuhakikisha wanarejea salama katika familia zao.
Kwa utayari wetu na ahadi thabiti ya kusudio hili jema, WWF inaleta mabadiliko chanya katika maisha ya wengi na kuleta matumaini ya mustakabali mzuri kwa watoto na familia zao.
Tunaamini kwamba hakuna familia inayopaswa kukabiliana na changamoto ya kupotea kwa mtoto peke yake.
Kauli Mbiu
"Kila Mtoto Anahesabika" Kauli hii inalenga kudumisha ustawi, usalama na haki za watoto.
Dhamira
Kupunguza visa vya kupotea na kuongeza nafasi ya kupatikana kwa mtoto anaepotea.
Maono
Kujenga usalama na mazingira yaliyo rafiki kwa watoto wote nchini Tanzania.
Programu Zetu
Mbinu Zetu: Kuzuia, Elimu, Kurejesha
Kushughulikia suala la watoto wanaopotea kunahitaji mbinu madhubuti na za kina, ambazo zinajumuisha sio tu juhudi za kuwapata watoto waliopotea bali pia kutoa msaada muhimu na rasilimali kwa familia zao na wanajamii wa karibu.
Ndiyo maana programu zetu zinaweka mkazo mkubwa kwenye juhudi za kuzuia upotevu, kutoa elimu, na kuhakikisha watoto wanarejea salama katika familia zao.
Kampeni ya Uhamasishaji
Lengo kuu la kampeni ya uhamasishaji ni kupunguza idadi ya watoto wanaopotea kwa kuelimisha umma kuhusu hatari na njia sahihi za kuzuia upotevu wa watoto. Kampeni inalenga kuunda hisia ya uwajibikaji kwa wazazi, walezi, vyombo vya usalama, na umma kwa ujumla, ili kuchukua hatua za kuzuia watoto kupotea na kuwasaidia kurejea salama nyumbani.
Kampeni hii inatoa vidokezo vya vitendo, rasilimali, na msaada wa kimsingi kwa lengo la kuwezesha watu binafsi na jamii kuchukua hatua za kuzuia upotevu wa watoto, pamoja na mwitikio wa haraka na ufanisi pindi mtoto anapopotea.
Jitihada za Dharura
Mpango wa jitihada za dharura kwa watoto waliopotea unalenga kutoa kipaumbele kwa utoaji wa taarifa za haraka na mifumo ya tahadhari, itifaki za wazi za mawasiliano, pamoja na juhudi za pamoja za utafutaji zinazoshirikisha watu wa kujitolea wenye mafunzo, vyombo vya dola, na wadau wengine.
Aidha, mpango huu unatoa msaada wa afya ya akili na rasilimali kwa familia za watoto waliopotea ili kusaidia kuongeza juhudi za utafutaji na kuongeza uwezekano wa kumpata mtoto.
Msaada Endelevu
Athari ya mtoto kupotea ni kubwa, siyo tu kwa mtoto lwenyewe hata kwa familia yake. Kutokuonekana kwa mtoto kunaweza kusababisha hisia mbaya, kuvuruga mwenendo wa familia, na kusababisha hata maradhi ya kimwili kama vile kukosa usingizi na kuongezeka kwa mafadhaiko. Hata baada ya mtoto kupatikana na kurudishwa nyumbani, changamoto za kihisia zinaweza kuendelea kuwepo. Kuumia kwa mtoto na athari za kihisia zinaweza kuwa ngumu kukabiliana nazo, kwa hiyo msaada endelevu ni muhimu sana kwa ajili ya uponyaji na kujenga upya.
Iwapo mtoto hajapatikana, msaada wa kitaalamu, pamoja na huduma za afya ya akili na kimwili, ni muhimu kusaidia familia kuishi kwa subira na kukabiliana na athari za kihisia. Ushauri nasaha na msaada wa kudumu ni muhimu kwa familia kukabiliana na hali hiyo.
Utafiti na Ripoti
Tutaendelea kuchambua mifumo iliyopo, kama vile sheria, sera, na mikakati inayohusiana na upotevu wa watoto nchini Tanzania na kimataifa. Tunaamini kwamba kwa kuchunguza na kuelewa sababu za msingi zinazochangia kuongezeka kwa kesi za watoto kupotea, tunaweza kuunda mikakati na sera madhubuti za kutatua tatizo hili na kuwalinda vyema watoto waishio Tanzania.
Mapitio ya Wapo Wapi Foundation

Mwaka 2014, nilishiriki katika Programu ya Mabalozi wa Kimataifa, na mwaka 2016/2017 niliteuliwa kuwa Bingwa wa Mabadiliko katika programu ya Empower Women ya UN Women. Pia, nimekuwa Mjumbe wa Amani kupitia Kikundi cha Vijana cha Amani ya Kimataifa (IPYG) na Mshauri wa Hult Prize On-campus kwa Afrika Mashariki mwaka 2018.
Nina ujuzi katika teknolojia ya habari, ikiwa ni pamoja na uchambuzi wa data. Nina shahada katika Usimamizi wa Ushirika na Uhasibu, na katika Utawala wa Fedha.
Kila kitu kilibadilika nilipokutana na tangazo la mtoto aliyepotea katika barabara ya Magomeni, eneo la karibu na ninapoishi. Tukio hili lilinifanya niungane na timu ya kutafuta mtoto huyo, na nilipofanya uchunguzi zaidi, niligundua kwamba watoto wengi nchini Tanzania hupotea kila mwaka, lakini kesi zao hazipewi uzito, haziripotiwi kwenye vituo husika, na mara nyingi zinasaulika.
Kwa hiyo, niliamua kuanzisha Taasisi ya Wapo Wapi Foundation (WWF) mwaka 2023 ili kuimarisha juhudi za kukabiliana na tatizo la upotevu wa watoto. Taasisi hii inatoa rasilimali na msaada kwa familia, na inalenga kujenga mazingira salama kwa watoto nchini Tanzania. Nina azma ya kuhamasisha wengine kujiunga na kampeni zetu za kulinda maisha ya watoto wanaopotea.